Kujiuzulu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza rasmi habari ya kujiuzulu waziri wake wa mambo ya nje.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Juba mji mkuu wa Sudan Kusini, serikali ya nchi hiyo ilitangaza jana Ijumaa kwamba Deng Alor Kuol, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amejiuzulu nafasi yake hiyo na kwamba amekuwa akiishi Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia tokea mwezi Februari mwaka huu. Ikitangaza habari hiyo bila kutoa maelezo zaidi, Wizara ya Habari ya Sudan Kusini imeongeza kwamba Deng Alor Kuol amekuwa akikataa kurejea Juba licha ya maombi na mashinikizo ya kumtaka afanye hivyo.
Hii ni katika hali ambayo serikali ya Sudan Kusini na waasi wa nchi hiyo wamepangiwa kukutana wiki ijayo huko Khartoum mji mkuu wa Sudan, kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo ya kurejesha amani ya kudumu nchini kwao, nchi ambayo imeharibiwa vibaya na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamekuwa yakiendelea nchini kwa muda mrefu. Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kufuatia uchochezi na uingiliaji wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi na hasa Marekani. Nchi hiyo changa tokea mwezi Disemba 2013 hadi sasa imekuwa uwanja wa mapigano kati ya wafausi wa Salvar Kiir, Rais wa Sudan na wa Riek Machar, Makamu wake wa zamani.