Mahasimu wa Sudan Kusini waonana ana kwa ana Khartoum
Mahasimu wawili wakubwa ambao ndio wahusika wakuu wa mgogoro wa miaka kadhaa sasa wa Sudan Kusini wameanzisha mazungumzo mpya ya amani ya kumaliza mgogoro wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Mazungumzo mengine ya ana kwa ana baina ya Rais Salva Kiir na hasimu wake mkubwa Riek Machar yameanza leo Jumatatu mjini Khartoum Sudan na kuhudhuriwa na Rais Omar al Bashir wa Sudan na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kukiwa na matumaini ya kupatikana utatuzi wa vita vya miaka minne na nusu sasa vya Sudan Kusini.
Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya mkutano wa siku ya Jumatano wa nchini Ethiopia kushindwa kutatua mgogoro huo. Viongozi wa Afrika Mashariki wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Sudan Kusini ambayo huenda ikalemewa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa iwapo mahasimu wa nchi hiyo watashindwa kukomesha umwagaji wa damu.
Makumi ya maelfu ya wananchi wameshauwa na karibu milioni nne wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo yaliyozuka mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua.
Mahasimu hao wawili walionana ana kwa ana siku ya Jumatano huko Addis Ababa Ethiopia baada ya kupita miaka miwili lakini pamoja na hayo walishindwa kufikia makubaliano. Serikali ya Sudan Kusini ilisema mara baada ya mkutano huo kuwa imechoshwa na Riek Machar.