Polisi nchini Zimbabwe yamtia mbaroni kiongozi wa upinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46356-polisi_nchini_zimbabwe_yamtia_mbaroni_kiongozi_wa_upinzani
Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe amekamatwa na polisi ya nchi hiyo baada ya kushinikiza kujiuzulu kwa mkuu wa Tume ya Uchaguzi, mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 26, 2018 15:28 UTC
  • Polisi nchini Zimbabwe yamtia mbaroni kiongozi wa upinzani

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe amekamatwa na polisi ya nchi hiyo baada ya kushinikiza kujiuzulu kwa mkuu wa Tume ya Uchaguzi, mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, Dakta Francis Danha, kinara wa chama cha upinzani cha Freedom Movement, ametiwa nguvuni na maafisa wa polisi alipokuwa katika mkutano wa vyama vya upinzani, ambapo alitoa mwito wa kujiuzulu Priscilla Chigumba, mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini humo NEC.

Amesikika akisema katika kanda ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba: "Hatutakubali Chigumba aendesha uchaguzi huu. Vyama vyote vya upinzani havikubaliana naye. Anapanga kuiba kura."

Haya yanajiri siku chache baada ya mlipuko uliotokea katika mkutano wa kisiasa wa Rais Emmerson Mnangagwa katika Uwanja wa White City katika mji wa Bulawayo.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Mlipuko huo ulitokea wakati Rais wa Zimbabwe akiondoka uwanjani hapo, baada ya kuwahutubia wafuasi wake, kuelekea uchaguzi mkuu wa Julai 30.

Mtu mmoja alifariki katika mripuko huo wa Jumamosi na wengine wawili wakiripotiwa kuaga dunia hapo jana kutokana na majeraha waliyoyapata, huku Rais Mnangangwa akinusurika na makamu wa rais Kembo Mohadi na wengine 48 wakijeruhiwa.

Rais Emmerson Mnangagwa alilitaja shambulizi hilo kama la kiwoga na kusisitiza kuwa mbinu hizo katu hazitafuta azma yake ya kuwania urais na kuwahudumia wananchi wa nchi hiyo maskini ya Kiafrika.