Mahasimu wa kisiasa nchini Sudan Kusini wakubaliana kusitisha vita
Mahasimu wawili wakubwa ambao ndio wahusika wakuu wa mgogoro wa miaka kadhaa sasa wa Sudan Kusini wameafikiana kusitisha mapigano huku wakikubaliana katika nukta nyingine kadhaa za kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliana waliyosaini jana Jumanne katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, Rais Salva Kiir na Riek Machar wameafikiana juu ya kuundwa miji mikuu mitatu nchini humo, ya Juba, Wau na Malakal, ambapo miji hiyo itakuwa makao makuu ya muda ya manaibu rais watatu watakaopendekezwa.
Wawili hao pia wamekubaliana kuiruhusu serikali ya Khartoum kulinda maeneo yenye utajiri wa mafuta nchini Sudan Kusini kwa kushirikiana na kushauriana na serikali ya Juba, sambamba na kuhuisha visima vya mafuta ili vizalishe kiwango cha hapo awali cha bidhaa hiyo.
Rais Omar al Bashir wa Sudan siku ya Jumatatu wakati wa kuanza mazungumzo hayo aliahidi kurejesha amani katika nchi hiyo jirani ili kufungua ukurasa mpya wa maendeleo katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Mazungumzo ya Jumatatu na jana Jumanne mjini Khartoum yamefanyika baada ya mkutano wa siku ya Jumatano iliyopita mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kushindwa kutatua mgogoro huo.
Makumi ya maelfu ya wananchi wameshauwa na karibu milioni nne wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo yaliyozuka mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo Riek Machar kuwa alipanga njama za kumpindua.