UN yapongeza nafasi ya Algeria katika mapambano dhidi ya ugaidi
Umoja wa Mataifa umeipongeza Algeria kwa nafasi yake katika mapambano dhidi ya ugaidi katika nchi za eneo la Sahel na magharibi mwa Afrika.
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika na katika eneo la Sahel barani humo amesisitiza udharura wa kustafidi na uzoefu wa Algeria katika vita hivyo dhidi ya ugaidi. Mohamed Ibn Chambas jana Jumanne alikuwa na mazungumzo huko Algiers mji mkuu wa Algeria na Abdelkader Messahel Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ambapo alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unapongeza hatua zinazotekelezwa na Algeria katika kuzisaidia nchi za magharibi mwa Afrika na za eneo la Sahel barani humo katika kupambana na ugaidi.
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa magharibi mwa Afrika na katika eneo la Sahel barani humo ameashiria pia kuhusu uzoefu wa Algeria katika kupambana na makundi ya kidini yenye misimamo ya kufurutu ada tangu mwanzoni mwa muongo wa 90 na kusisitiza kuwa kuna udharura wa kustafidi na uzoefu huo uliotajwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama katika eneo.