UN: Jeshi la Mali liliua raia12 katika ulipizaji kisasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46398-un_jeshi_la_mali_liliua_raia12_katika_ulipizaji_kisasi
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA kimesema wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika waliuawa raia 12 katika operesheni ya kulipiza kisasi mwezi uliopita, baada ya mwenzao kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2018 09:50 UTC
  • UN: Jeshi la Mali liliua raia12 katika ulipizaji kisasi

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA kimesema wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika waliuawa raia 12 katika operesheni ya kulipiza kisasi mwezi uliopita, baada ya mwenzao kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.

Taarifa ya kikosi hicho imesema kuwa, watu wasiojulikana walimuua mwanajeshi wa Mali mnamo Mei 19 kwa kumfyatulia risasi katika soko la mifugo la kila wiki la Boulkessy, ambapo askari wenzake walifanya operesheni ya kulipiza kisasi kifo cha mwenzaona wakaishia kuua raia 12.

Kikosi hicho cha UN kimesema tayari kimeikabidhi serikali ya Bamako ripoti ya uchunguzi wake kuhusiana na tukio hilo, ingawaje maafisa wa serikali hawajatoa taarifa yoyote kuhusu kadhia hiyo hadi sasa.

Jeshi la Mali limekuwa likikabiliwa na tuhuma za kuua raia katika operesheni zao mbalimbali. Wiki iliyopita mashirika ya kiraia nchini humo yakiongozwa na Fulani Association Tabital Pulaku yalifichua habari ya kuuawa raia 25 na wanajeshi wa Mali katika operesheni ya wiki mbili zilizopita, dhidi ya magenge ya kigaidi yenye mfungamano na al-Qaeda, katika kijiji cha Nantaka, jimbo la Mopti.

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA

Serikali ilithibitisha kugundua makaburi matatu ya umati katika eneo hilo ambapo raia hao waliuawa na kisha kuzikwa na wanajeshi hao, huku Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Tiena Coulibaly, akisema wameanzisha uchunguzi kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Askari wa Umoja wa Mataifa na wa Ufaransa walitumwa nchini Mali mwaka 2013 lakini wameshindwa kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.