Jun 29, 2018 07:19 UTC
  • Rais wa Ghana awafuta kazi wakuu wa tume ya uchaguzi

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amempiga kalamu nyekundu Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Charlotte Osei kutokana kile alichotaja kama utovu wa nidhamu na utepetevu.

Mustapha Abdul-Hamid, Waziri wa Habari wa Ghana amesema Rais Akufo-Addo amewafuta kazi pia manaibu wawili wa Osei, kwa msingi wa mapendekezo yaliyotolewa na kamati maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya wakuu hao wa chombo hicho cha kusimamia uchaguzi.

Hata hivyo upinzani nchini humo unashikilia kuwa, madai dhidi ya mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi na manaibu wake ni bandia.

Osei aliteuliwa katika wadhifa huo na rais wa zamani wa nchi hiyo John Dramani Mahama, katikati ya mwaka 2015, na akaendesha vizuri uchaguzi wa mwaka 2016.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi aliyetimuliwa, Charlotte Osei

Katika uchaguzi huo wa Disemba mwaka 2016, Akufo-Addo alipata ushindi kwa kuzoa asilimia 53.8 ya kura na kumbwaga Rais wa wakati huo John Dramani Mahama, aliyezoa asilimia 44.4 ya kura zote. 

Uchaguzi ujao katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika unatazamiwa kufanyika Disemba mwaka 2020, ambapo mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya chama tawala cha New Patriotic Party na chama kikuu cha upinzani cha National Democratic Congress. 

Tags