Mashinikizo ya Saudia yapelekea Nigeria isimuachilie huru Sheikh Zakzaky
Utawala wa Saudi Arabia unaishinikiza serikali ya Nigeria isimuachilie huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Kwa mujibu wa tovuti ya Al Akhbar ya Lebanon, pamoja na kuwa imepita miezi 19 tokea Mahakama ya Nigeria itoe hukumu ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky, lakini kiongozi huyo wa Kiislamu hajaachiliwa huru kutokana na mashinikizo ya Saudia.
Tovuti hiyo imeandika kuwa Sheikh Zakzaky anashikiliwa katika kizuizi cha shirika la usalama wa taifa nchini humo. Ripoti hiyo imesema Sheikh Zakzaky ambaye kesi yake ilikuwa isikilizwe jana imeahirishwa hadi Agosti pili kutokana na mshtuko wa ubongo aliopata ambao umepelekea hali yake ya kiafya iwe mbaya zaidi.
Ikumbukwe kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alikamtwa baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya yeye na mke wake mwezi Disemba 2015 wakati jeshi la nchi hiyo lilipovamia Husainia ya Baqiyyatullah mjini Zaria na kuua kwa umati mamia ya Waislamu.
Watoto wa Sheikh Zakzkay ni miongoni mwa mamia ya Waislamu waliouliwa shahidi na kujeruhiwa na wanajeshi wa Nigeria katika jinai hiyo.
Hivi sasa miaka miwili na nusu imepita tangu kutokea uvamizi huo lakini serikali ya Nigeria ingali inang'ang'ania kumshikilia korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky licha ya kuwa mwaka 2016 Mahakama Kuu ya nchi hiyo ilitoa amri ya kuachiliwa huru.