Algeria yasitisha kuwafukuzia katika jangwa la Sahara wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46796-algeria_yasitisha_kuwafukuzia_katika_jangwa_la_sahara_wakimbizi
Algeria karibuni imesimamisha kuwafukuza wakimbizi kuelekea katika jangwa la Sahara baada ya hatua hiyo kupingwa vikali na maafisa kadhaa wa usalama wa ngazi ya juu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2018 09:23 UTC
  • Algeria yasitisha kuwafukuzia katika jangwa la Sahara wakimbizi

Algeria karibuni imesimamisha kuwafukuza wakimbizi kuelekea katika jangwa la Sahara baada ya hatua hiyo kupingwa vikali na maafisa kadhaa wa usalama wa ngazi ya juu.

Mwezi uliopita shirika la habari la Associated Press liliwanukuu maafisa wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) wakieleza kuwa maafisa wa Algeria tangu mwezi Mei mwaka jana wamewatelekeza watu zaidi ya 13,000 wakiwemo wanawake na watoto katika mipaka ya jangwa hilo linalopakana na Algeria, Niger na Mali.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Algeria ilikuwa ikiwalazimisha karibu kila wiki  mamia ya wakimbizi kuelekea jangwani; hatua ambayo wakati mwingine imesababisha vifo vya wakimbizi. Pamoja na kutolewa taarifa hiyo lakini serikali ya Algeria imekataa kutoa maelezo kuhusu tukio hilo.

Fukuzafukuza hiyo ya wakimbizi ya serikali ya Algeria imetekelezwa huku Umoja wa Ulaya ukizishinikiza serikali za  kaskazini mwa Afrika kuzuia wimbi la wakimbizi wanaojaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.

Wakimbizi wa Kiafrika katika safari ya kuelekea Ulaya 
 

Wakati huo huo taarifa nyingine zinasema kuwa Algeria inaendelea kuwatia mbaroni wakimbzi kwa umati lakini wakimbizi hao wakiwemo wanawake wajawazito wanahifadhiwa katika jela zenye mrundikano wa watu. Mkuu wa usalama wa taifa na wa vikosi vya usalama wa Algeria walifukuzwa kazi baada ya kufichuka ripoti hii kuhusu kutelekezwa wakimbizi katika jangwa la Sahara.