Eritrea na Somalia zasaini makubaliano ya kuhuisha uhusiano kati ya pande mbili
Serikali ya Eritrea imetangaza kuwa imesaini makubaliano na Somalia kwa lengo la kuhuisha uhusiano wa kidiplomasia na kubadilishana mabalozi kati ya nchi mbili hizo.
Serikali ya Eritrea imesema kuwa imesaini makubaliano hayo na Somalia chini ya anwani ya "Azimio la Uhusiano wa Kidugu."Serikali ya Eritrea imesema katika taarifa yake kuwa Rais Isaias Afwerki wa nchi hiyo na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo ndio waliosaini makubaliano hayo yanayosisitiza kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia na kubadlishana mabalozi kati ya nchi mbili.
Rais wa Somalia Jumamosi iliyopita alifanya ziara huko Asmara mji mkuu wa Eritrea baada ya kupita miaka 15 tangu nchi yake ikate uhusiano na Eritrea. Hivi karibuni Eritrea ilisaini makubaliano ya suluhu na kurejesha uhusiano na Ethiopia pia na hivyo kuhitimisha mzozo na uhasama uliokuwepo kati ya pande mbili hizo kwa muda wa miaka 20.