Umoja wa Mataifa waongeza muda wa kuhudumu AMISOM nchini Somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa kuhudu wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, AMISOM, nchini Somalia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress amesema, hatua hii imekuja baada ya kubainika kuwa, wanajeshi wa Somalia bado hawajapata mafunzo ya kutosha kuachiwa usalama wa nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa una wanajeshi 1,000 ambao wanashirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Afrika AMISOM wapatao 21,000 ambao wanapambana na magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab.
Guteress ameliandikia barua Baraza la Usalama na kuliambia kuwa, haitawezekena tena kuwapunguza wanajeshi wa AMISOM kufikia mwezi Oktoba kama ilivyopangwa.
Hatua hii imesababisha baraza hilo kuamua kuwa wanajeshi hao wa AMISOM sasa waondoke nchini humo kufikia tarehe 31 mwezi Mei mwaka 2019. Mamia ya watu wamepoteza maisha mwaka huu pekee katika mashambulizi ya kundi la magaidi wakufurishaji wa Al Shabab.

Awali Umoja wa Mataifa ambao unafadhili askari hao wa AMISOM ulikuwa umetaka kuanzishwe operesheni ya kupunguza askari hao ambao sasa ni 21,000. Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.