Wanajeshi 3 Wasomali wauawa katika hujuma ya kigaidi nje ya Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47248-wanajeshi_3_wasomali_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_nje_ya_mogadishu
Wanajeshi wasiopungua watatu wa Somalia wameuawa kufuatia hujuma ya kigaidi katika wilaya ya Afgoye iliyo kilomita 30 kaskaini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Aug 05, 2018 15:33 UTC
  • Wanajeshi 3 Wasomali wauawa katika hujuma ya kigaidi nje ya Mogadishu

Wanajeshi wasiopungua watatu wa Somalia wameuawa kufuatia hujuma ya kigaidi katika wilaya ya Afgoye iliyo kilomita 30 kaskaini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.

Taarifa zinasema hujuma hiyo imetekelezwa na kundi la magaidi wakufurishaji wa Al Shabab ambao wamelenga wanajeshi wa Somalia waliofika eneo la Afgoye wiki hii kuimarisha usalama kabla ya safari tarajiwa ya Rais Mohammad Abdullahi Farmaajo.

Maafisa wa usalama wanasema walifyatulia risasi gari la magaidi ambalo lilikuwa limesheheni bomu kabla ya kulipuka ambapo wanajeshi watatu walipoteza maisha.

Kundi la kigaidi la Al Shabab limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi na kusema idadi ya waliouawa ni zaidi ya inayotangazwa.

Abdiasis Abu Musab, msemaji wa Al Shabab amenukuliwa na Shirika la Habari la Reuters akidai kuwa ni wanajeshi 11 waliouawa katika hujuma hiyo.

Hayo yanajiri siku chache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa kuhudumu wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, AMISOM, nchini Somalia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress amesema, hatua hii imekuja baada ya kubainika kuwa, wanajeshi wa Somalia bado hawajapata mafunzo ya kutosha kuachiwa usalama wa nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa una wanajeshi 1,000 ambao wanashirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Afrika AMISOM wapatao 21,000 ambao wanapambana na magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab.

Hatua hii imesababisha baraza hilo kuamua kuwa wanajeshi hao wa AMISOM sasa waondoke nchini humo kufikia tarehe 31 mwezi Mei mwaka 2019. Mamia ya watu wamepoteza maisha mwaka huu pekee katika mashambulizi ya kundi la magaidi wakufurishaji wa Al Shabab.