Wanamgambo 52 wauawa Sinai Misri
(last modified Sun, 05 Aug 2018 15:41:40 GMT )
Aug 05, 2018 15:41 UTC
  • Wanamgambo 52 wauawa Sinai Misri

Jeshi la Misri limetangaza kuwa limefanikiwa kuua wanamgambo 52 katika siku za hivi karibuni kwenye eneo la kaskazini mwa Rasi ya Sinai.

Rasi ya Sinai iko kaskazini mwa Misri na jeshi la nchi hiyo limetangaza leo Jumapili kuwa mbali na kuua wanamgambo 52, limefanikiwa pia kuwatia mbaroni wanamgambo wengine 49 na kuangamiza maficho 26 ya silaha pamoja na vifaa 64 vya miripuko.

Jeshi hilo limeongeza kuwa, ndege za kivita za jeshi hilo zimeangamiza magari 32 yaliyokuwa na silaha katika jangwa la magharibi mwa Misri.

Wanajeshi wa Misri katika operesheni maalumu kaskazini mwa nchi hiyo

 

Kwa upande wake shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa ni jambo lisiloyumkinika kuthibitisha taarifa hiyo kutokana na kwamba ni vigumu kulifikia eneo la kaskazini mwa Rasi ya Sinai.

Wakati huo huo gazeti la al Misri al Yaum leo limezinukuu duru za usalama za Misri zikisema kuwa, magaidi 11 wameuawa katika mapigano yaliyotokea baina ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo katika eneo la al Arish la mkoa wa Sinai Kaskazini.

Mkoa wa Sinai Kaskazini ni kituo kikubwa cha mashambulizi ya magenge yenye silaha hususan magaidi wanaojiita kwa jina la Wilaya ya Sinai, ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS). 

Kundi hilo limesababisha madhara mengi kwa jeshi la polisi wa Misri katika eneo la Sinai.

 

Tags