Aug 09, 2018 08:02 UTC
  • Kuteuliwa Ramazani Shadary kumrithi rais Kabila kunaweza kuakhirisha uchaguzi Kongo DR

Wasiwasi wa kuahirishwa uchaguzi mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeongezeka zaidi, siku moja tu baada ya chama tawala cha Rais Joseph Kabila kumtangaza Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mbeba bendera ya chama hicho pamoja na vyama tanzu katika uchaguzi huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wasiwasi huo umeongezeka kutokana na kuwa, Emmanuel Ramazani Shadary mwenye umri wa miaka 57 na ambaye amewahi kushika nyadhifa kama ya Waziri wa Mambo ya Ndani anakabiliwa na tuhuma mbalimbali.

Baadhi ya duru zinasema kuwa, tuhuma anazokabiliwa nazo kama ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu huenda zikakwamisha juhudi zake za kutaka kumrithi Rais Kabila na hivyo kupelekea uchaguzi huo kuakhirishwa. Aidha Ramazani Shadary ni miongoni mwa wanasiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliowekewa vikwazo na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya.

Rais Joseph Kabila hatogombea kiti cha urais katikka uchaguzi ujao wa Disemba

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kutangazwa Ramazani Shadary kuwa mgombea Urais kunaweza kuvuruga mwenendo wa uchaguzi huo na hivyo kupelekea kuakhirishwa.

Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umepangwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu. Mbali na chama tawala, vyama viwili vikuu vya upinzani nchini humo vimeshatangaza wagombea wao watakaochuana na mgombea wa chama cha Rais Kabila.

Jean-Pierre Bemba, mwenye umri wa miaka 55 na hasimu wa Rais Kabila ambaye alirejea Kinshasa wiki iliyopita baada ya kuondolewa mashtaka ya uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ameshakabishi fomu zake kwa Tume ya Uchaguzi. Mgombea mwingine wa upinzani ni Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS).

Tags