Aug 22, 2018 02:50 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani shambulio la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani shambulio la kigaidi la kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria ambalo lilipelekea kuuawa makumi ya raia wasio na hatia.

Antonio Guterres sambamba na kulaani shambulio hilo la kigaidi ametoa wito wa kutiwa mbaroni na kupandishwa kizimbani wale wote waliohusika na jinai hiyo dhidi ya binadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea pia wasiwasi mkubwa alionao wa kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji katika eneo la Ukanda wa Ziwa Chad na kusisitiza juu ya udharura wa kufanyika juhudi maradufu za kukabiliana na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Aidha Antonio Guterres amebainisha juu ya udharura uliopo kkwa bara la Afrika kufanya juhudi za kurejesha amani na utulivu katika maeneo yanayokabiliwa na vurugu na machafuko.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Kundi la kigaidi la Boko Haram Jumapili usiku lilishambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua makumi ya raia sambamba na kuchoma moto baadhi ya nyumba za vijiji hivyo.

Mashambulio ya kundi hilo nchini Nigeria na katika baadhi ya nchi jirani yaliyoanza mwaka 2009, hadi sasa yameshasababisha watu zaidi elfu 20 kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita kupoteza makazi na kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

Juhudi za serikali ya Nigeria za kuliangamiza kundi hilo la kigaidi hadi sasa hazijapata mafanikio kamili licha ya kushirikiana na nchi za eneo kukabiliana na wanamgambo hao.

Tags