Libya yajiweka katika hali ya tahadhari kufuatia mripuko wa kipindupindu nchini Algeria
Wizara ya Afya ya Libya imetangaza kuwa hali ya tahadhari imetangazwa nchini humo kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu kufuatia mripuko wa ugonjwa huo uliotokea katika nchi jirani ya Algeria.
Wizara ya Afya ya Libya imeeleza kupitia taarifa kuwa imeongeza kiwango cha tahadhari na utayari wa kukabiliana na uwezekano wa kuzuka mripuko wa kipindupindu kutokea ulikoanzia nchini Algeria hususan katika maeneo ya mpaka wa pamoja wa nchi mbili.
Wizara hiyo aidha imevitaka vituo vya tiba na hospitali kuwa na tahadhari kwa kuchunguza hali za watu wanaoingia nchini humo kutokea Algeria kuona kama wana ishara za ugonjwa huo.
Maafisa wa tiba nchini Algeria walitangaza jana kuwa idadi ya watu waliothibitika kukumbwa na ugonjwa na kipindupindu katika mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo imeongezeka.
Wizara ya Afya ya Algeria imetangaza kuwa watu 147 wanashukiwa kukumbwa na ugonjwa huo huku wengine 49 wakiwa wamethibitika na kulazwa katika hospitali za kaskazini mwa nchi hiyo.../