Amnesty International yalalamikia kutiwa nguvuni Waislamu nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47801-amnesty_international_yalalamikia_kutiwa_nguvuni_waislamu_nchini_nigeria
Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limelaani hatua ya serikali ya Abuja ya kuwaweka kizuizini kinyume sheria Waislamu hasa wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2018 23:26 UTC
  • Amnesty International yalalamikia kutiwa nguvuni Waislamu nchini Nigeria

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limelaani hatua ya serikali ya Abuja ya kuwaweka kizuizini kinyume sheria Waislamu hasa wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Amnesty International ilitoa taarifa hiyo jana na mbali na kulalamikia kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria wananchi wa Nigeria kwa tuhuma zisizo na uthibitisho kama madai ya kujihusisha na vitendo vya kigaidi au kuwa wafuasi wa mrengo unaotaka kujitenga eneo la Biafra imesema kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, maelfu ya wananchi wametiwa mbaroni kwa madai hayo na pia kwa madai ya kuwa wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Amnesty International, wanachama 600 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hawajulikani walipo hadi hivi sasa na kwa miaka kadhaa sasa familia nyingi zimekuwa zikitafuta jamaa zao bila ya mafanikio.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aliyewekwa kizuizini na serikali 

 

Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya mwaka 2015 na jeshi la Nigeria kabla ya kutiwa mbaroni. Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru, lakini hadi hivi sasa serikali ya nchi hiyo inakataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama.

Katika kipindi chote hiki, wananchi wa Nigeria wamekuwa wakifanya maandamano katika miji tofauti wakishinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Shirika la Amnesty International limeionya serikali ya Nigeria kuhusu hatari za kuendelea kuwatia mbaroni raia kwa madai tofauti kama ya kuhusika na vitendo vya ugaidi au kuwa wanachama wa mrengo unaopigania kujitenga eneo la Biafra.