Kamanda wa Jeshi la Libya adai, jeshi la Algeria limeivamia Libya
Kamanda wa jeshi la taifa la Libya amedai kuwa Algeria imeingiza wanajeshi wake katika ardhi ya nchi hiyo.
Jenerali Khalifa Haftar amedai kuwa wanajeshi kadhaa wa Algeria wameingia katika ardhi ya Libya na iwapo hali ya mambo itaendelea kuwa hivi Libya itahamishia vita ndani ya Algeria. Vitisho hivyo vya Jenerali Haftar vimeakisiwa pakubwa na vyombo vya habari vya Algeria.
Wakati huo huo gazeti la al Nahar limejibu matamshi hayo ya Jenerali Khalifa Haftar kwa kuandika kuwa Haftar ametoa matamshi hayo ikiwa ni katika kampeni za uchaguzi unaotazamiwa kufanyika nchini Libya.
Ripoti ya gazeti hilo la Algeria limeongeza kuwa, Algeria inafuata siasa za kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Hii si mara ya kwanza ambapo Jenerali Khalifa Haftar kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya anaikosoa Algeria. Kamanda huyo wa Libya Novemba mwaka 2014 pia aliwahi kusema kuwa Tunisia, Algeria, Mali na Chad zinahitaji maliasili za Libya na kwamba nchi hizo zinakodolea jicho la tamaa utajiri wa mafuta na gesi ya nchi hiyo.