Rais Muhammad Buhari atangaza kutetea kiti chake katika uchaguzi ujao wa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48106-rais_muhammad_buhari_atangaza_kutetea_kiti_chake_katika_uchaguzi_ujao_wa_nigeria
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametangaza kuwa atagombea tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Februari mwaka ujao wa 2019.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2018 03:02 UTC
  • Rais Muhammad Buhari atangaza kutetea kiti chake katika uchaguzi ujao wa Nigeria

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametangaza kuwa atagombea tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika Februari mwaka ujao wa 2019.

Muhammadu Buhari mwenye umri wa miaka 75 amesema hayo katika makao makuuu ya chama tawala katika mji mkuu wa Nigeria Abuja ambapo alikabidhi rasmi pia fomu za uteuzi wa chama kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.

Buhari ambaye aliingia madarakani mwaka 2015 kwa ahadi za kutokomeza ufisadi nchini Nigeria ambayo ni kubwa kiuchumi na wingi wa idadi ya watu barani Afrika amekuwa akikosolewa mno na wapinzani wake kutokana na kile wanachosema kuwa, ameshindwa kutekeleza ahadi zake.

Wanamgambo wa Boko Haram

Aidha wapinzani wa Rais Buhari wanasema kuwa, kiongozi huyo ameshindwa kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram kwani moja ya ahadi zake kuu katika kampeni za uchaguzi ilikuwa ni kukabiliana na magaidi hao ambao wamesababisha maafa makubwa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrikka na hata katika nchi jirani kama Cameroon, Niger na Chad.

Chama tawala nchini Nigeria cha APC bado hakijatangaza tarehe ya kuanza kuchambua sifa za watangaza nia ya kugombea urais na hatimaye kumtangaza mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi ujao wa Rais.

Wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kwamba, serikali ya Rais Buhari haina azma na irada kama ya kupambana na magaidi. Kwa sasa uchumi wa Nigeria unalegalega, ukosefu wa ajira na umasikini vimeongezeka huku kukiwemo na tatizo kubwa la ufisadi.