Sep 17, 2018 02:22 UTC
  • Magaidi kadhaa wa Boko Haram wauliwa na jeshi la Nigeria, Borno

Wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram wameuawa katika operesheni iliyofanywa jana Jumapili na wanajeshi wa Nigeria katika jimbo la Borno, la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Katika taarifa yake, jeshi la Nigeria bila ya kutaja idadi kamili limesema "Kikosi cha 222 cha jeshi letu kimepambana na wanachama wa Boko Haram mjini Maiduguri, karibu na eneo la Bama na magaidi kadhaa wameuawa na wengine wamefanikiwa kutoroka wakiwa na majeraha ya risasi."

Picha zilizosambazwa na jeshi la Nigeria katika mtandao wa kijamii wa Twitter zinaonesha miili ya magaidi hao ikiwa imerundikana kandokando ya barabara.

Operesheni ya Upinde

Kadhalika silaha kadhaa za magaidi hao wakufurishaji zimepatikana katika operesheni hiyo iliyopewa jina la Upinde, ambayo ni sehemu ya operesheni pana ya Lafiya Dole (yaan amani kwa njia zote).

Operesheni ya jana imefanyika siku moja baada ya watu wasiopungua wanane kuuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria katika shambulizi la kundi la kigaidi la Boko Haram.

Kundi hilo la kigaidi lilianzishwa mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria na hadi hivi sasa limeshaua zaidi ya watu 20 elfu huko Nigeria na katika nchi jirani na limeshapelekea zaidi ya watu milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.

Tags