Sep 21, 2018 03:23 UTC
  • Watu 9 wauawa katika shambulio la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi la kigaidi la Boko Haram limeendelea kufanya mauaji kaskazini mashariki mwa Nigeria ambapo watu 9 wanaripotiwa kuuawa kufuatia shambulio la magaidi hao.

Duru za usalama zinaripoti kuwa, watu tisa wameuawa baada ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram kushambuulia vijiji viwili katika mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Watu kadhaa wanaripotiwa kujeruhiwa pia katika shambulio hilo huku magaidi hao wa Boko Haram wakivichoma moto kikamilifu vijiji hivyo viwili.

Shambulio hilo la Boko Haram linaripotiwa katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni magaidi hao wameshadidisha mashambulio yao dhidi ya ngome za jeshi na makazi ya raia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Shambulio la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi hilo la kigaidi lilianzisha uasi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria na hadi hivi sasa limeshaua zaidi ya watu 20 elfu nchini humo na katika nchi jirani na limeshapelekea zaidi ya watu milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ameendelea kukosolewa kutokana na kutotekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni ambapo moja ya ahadi hizo ilikuwa ni kulitokomeza kundi la kigaidi la Boko Haram.

Hata kuundwa kikosi cha pamoja cha nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger kwa ajili ya kupambana na Boko Haram bado hakujafanikiwa kulisambaratisha kundi hilo ambalo limeeneza harakati zake nje ya mipaka ya Nigeria.

Tags