China: Hatuna azma ya 'kuikoloni' Zimbabwe licha ya kushindwa kutulipa madeni yetu
China imesema Beijing haina nia wala mpango wa kunyakua na kudhibiti mali za Zimbabwe licha ya serikali ya Harare kushindwa kuilipa nchi hiyo malimbikizo ya madeni yake.
Gazeti la Independent la Zimbabwe limemnukuu mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa China akisema kuwa, katu nchi hio ya Asia haijaazimia kufanya ukoloni mamboleo barani Afrika kama yalivyofanya mataifa ya Ulaya katika karne ya 19.
Amebainisha kuwa, "Nchi za Magharibi ndizo zinazoendesha propaganda kwamba China inataka kuyakoloni mataifa ya bara Afrika kwa kushindwa kulipa madeni ya Beijing, ili kuifanya nchi hiyo ya Asia ichukiwe barani humo."
Inaarifiwa kuwa, Harare inadaiwa malimbikizo ya dola milioni 300 na Beijing, kutokana na mikopo iliyopewa na China huko nyuma.
Hivi karibuni, duru za habari ziliarifu kuwa, China inadhibiti Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Zambia pamoja na Shirika la Utangazaji la nchi hiyo ya Kiafrika, baada ya kushindwa kulipa malimbikizo ya deni kwa serikali ya Beijing.
Mapema mwaka huu, Rais Xi Jinping akihutubu katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa tatu wa Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika (Focac) sambamba na kuashiria juu ya umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa Beijing na bara hilo alisema kuwa, China itazisaidia nchi za bara hilo katika nyanja zote na kwamba inapendelea kuona uhusiano huo ukistawi zaidi.
Akiashiria juu ya uungaji mkono mpya wa kifedha wa kiasi cha dola bilioni 60 wa China kwa bara la Afrika amesema kuwa, uungaji mkono huo utafanyika katika sura ya misaada ya serikali, uwekezaji, udhamini wa fedha kupitia taasisi na mashirika katika uwanja wa kustawisha miundombinu.