Afrika Kusini yatuhumiwa kushirikiana na Saudia katika mauaji ya watu wa Yemen
Serikali ya Afrika Kusini imetuhumiwa kuwa inashirikiana na Saudi Arabia katika mauaji yanayofanywa na utawala huo wa kifalme dhidi ya raia wasio na hatia nchini Yemen.
Hayo yameelezwa na jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu baada ya Riyadh na Abu Dhabi kutia saini mikataba ya kununua silaha kutoka Afrika Kusini yenye thamani ya dola bilioni 20. Duru za kuaminika zinasema silaha hizo zinatumiwa katika vita na mashambulizi yanayofanywa na Saudia na Imarati dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini mwezi Julai mwaka huu alikamilisha safari yake katika nchi za Saudi Arabia na Imarati kwa kutia saini mikataba ya mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 20, suala mbalo lilizusha maswali mengi kuhusu sababu na siri ya mauzo ya kiwango hicho kikubwa cha silaha.

Ripoti za kuaminika sinasema kuwa, mauzo ya silaha za Afrika Kusini kwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi yamekuwa yakiongozeka tangu mwanzoni mwa vita vya Saudi Arabia na Imarati dhidi ya taifa la Yemen mwaka 2015.
Mtandao wa Media Review wa Afrika Kusini umeandika katika ripoti yake iliyobeba kichwa cha maneno: Jinai za Kivita Yemen: Zimetengenezwa Afrika Kusini" kwamba licha ya uharibifu mkubwa na mgogoro wa kibinadamu uliosababishwa na mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen, nchi kadhaa ikiwemo Afrika Kusini zinaendelea kuiuzia silaha Saudia na waitifaki wake.
Mtandao huo umeandika kuwa: Mbali na Marekani na Uingereza zinazoongoza katika orodha ya nchi zinazozipa silaha kwa wingi Saudi Arabia na waitifaki wake katika vita vya Yemen, Afrika Kusini pia inafanya jitihada kubwa za kufaidika na vita hivyo, suala linaloiweka katika orodha ya nchi zinazoshiriki katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Yemen.
Maelfu ya raia wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi huko Yemen kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.