Upizani Zimbabwe: Rais Mnangagwa hana uhalali wa kuongoza
Kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa ametoa mwito wa kuundwa Mamlaka ya Kitaifa ya Mpito akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro kuhusu uhalali wa serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa.
Katika kikao na waandishi wa habari hapo jana Jumanne, Chamisa ambaye chama chake kimekataa kata kata kutambua ushindi wa Mnangagwa katika uchaguzi wa urais wa Julai 30, amesema serikali ambayo sio halali haina uwezo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo.
Amesema kuundwa Mamlaka ya Kitaifa ya Mpito ndilo jambo pekee litakaloifanya nchi hiyo isiendelee kutengwa na jamii ya kimataifa.
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye ametoa wito wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya vyama vya siasa kwa ajili ya kujenga upya uchumi wa nchi hiyo, anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukomesha hali ya kutengwa Zimbabwe kimataifa na kurekebisha uchumi unaoyumbayumba kutokana na ukosefu wa ajira na uhaba wa fedha za kigeni.

Mwezi uliopita, wabunge wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) kinachoongozwa na Nelson Chamisa walimzomea Rais Mnangagwa alipoanza kusoma hotuba yake kabla ya kususia hotuba hiyo na kuondoka bungeni.
Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge hao wa MDC walisikika wakiimba nyimbo zinazokishutumu chama tawala cha ZANU-PF, wakisisitiza kuwa rais huyo haheshimu utawala wa sheria.