Mbunge auawa katika mripuko wa bomu Mogadishu, Somalia
Polisi ya Somalia imesema mbunge mmoja wa eneo la HirShabelle amepoteza maisha katika mripuko wa bomu uliotokea adhuhuri ya leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
Kapteni Muhammad Yusuf, ofisi wa ngazi ya juu wa polisi katika eneo hilo amesema mbunge huyo wa bunge la kieneo anayejulikana kwa jina Abdiweli Mohamed Ibrahim ameuawa hii leo katika mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari lake, karibu na lango kuu la Mgahawa wa Londo, wilayani Hamarweyne.
Mbunge huyo ameuawa katika mripuko wa bomu siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar kuwasili katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa ajili ya ziara ya siku mbili, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia.

Ingawaje hadi hivi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mripuko huo wa leo, lakini genge la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara haswa dhidi ya maafisa wa serikali, wanasiasa, maafisa usalama na wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Katikati ya mwezi uliopita, watu 20 waliuawa na wengine 40 walijeruhiwa katika miripuko miwili ya mabomu iliyopishana kwa dakika chache tu, katika mji wa Baidoa wa kusini magharibi mwa Somalia.
Magaidi wakufurishaji wa al-Shabaab wenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wanaendesha kampeni ya mauaji kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia yenye makao yake Mogadishu na ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.