Waislamu Nigeria waendeleza maandamano kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49582-waislamu_nigeria_waendeleza_maandamano_kutaka_sheikh_zakzaky_aachiliwe
Waislamu nchini Nigeria wameendeleza maandamano katika mji mkuu, Abuja, kulalamikia kuendelea kushikiliwa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 17, 2018 23:15 UTC
  • Waislamu Nigeria waendeleza maandamano kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe

Waislamu nchini Nigeria wameendeleza maandamano katika mji mkuu, Abuja, kulalamikia kuendelea kushikiliwa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Sheikh Zakzaky ambaye ni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) na mke wake,wamekuwa kizuizini tangu mwezi Disemba mwaka 2015 na wanakabiliwa na tuhuma za mauaji, kuitisha mkusanyiko kinyume cha sheria, kuvuruga amani ya nchi na nyinginezo. Sheikh Zakzaky amekanusha tuhuma zote hizo.

Idadi kubwa ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky walikamatwa wakati jeshi na vikosi vya ulinzi vya Nigeria vilipofanya jinai na ukandamizaji mkubwa dhidi ya ofisi za Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN).

Wanawake katika maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Katika jinai hiyo, jeshi la Nigeria liliua kwa umati karibu wafuasi 1000 wa Sheikh Zakzaky wakiwemo wanawe watatu na baadaye kuwazika katika makaburi ya umati. Sheikh Zakzaky na mkewe walipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammad Buhari licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru.

Wiki iliyopita pia Waislamu Nigeria wameandamana nje ya ofisi za Tume ya Haki za Binaadamu katika mji mkuu Abuja, kulaani mauaji yaliyofanyika kati ya 27 hadi 30 Oktoba mwaka huu.