Kiongozi wa upinzani Rwanda: Mashinikizo hayataninyamazisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49977-kiongozi_wa_upinzani_rwanda_mashinikizo_hayataninyamazisha
Mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mashuhuri wa Rais Paul Kagame wa Rwanda Diane Shima Rwigara amesema katu hatasalimu amri mbele ya mashinikizo na vitisho dhidi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2018 12:59 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Rwanda: Mashinikizo hayataninyamazisha

Mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mashuhuri wa Rais Paul Kagame wa Rwanda Diane Shima Rwigara amesema katu hatasalimu amri mbele ya mashinikizo na vitisho dhidi yake.

Rwigara ambaye kesho Alkhamisi anatazamiwa kufika mahakamani kusikiliza mashitaka yanayomkabili ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, hakuna aina au kiasi chochote cha mashinikizo kitamfanya afumbie macho na kunyamazia kimya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Rwanda.

Hii ni katika hali ambayo, kiongozi huyo wa upinzani ambaye amekuwa akikosoa serikali ya Rais Kagame wazi wazi huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 22 jela iwapo atapatikana na hatia katika mashitaka yanayomkabili.

Mapema mwezi Oktoba, Rwigara pamoja na mama yake waliachiwa huru kwa dhamana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Rwanda, lakini walitakiwa kutotoka katika mji mkuu Kigali mbali na kukabidhi pasi zao za kusafiria kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali.

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Wawili hao wanadaiwa kukwepa kulipa kodi zinazoihusu kampuni ya tumbaku inayomilikiwa na familia yao; lakini kabla ya hapo, Diane Rwigira alituhumiwa kughushi na kufanya udanganyifu katika fomu alizojaza kwa ajili ya kugombea urais mwezi Agosti mwaka jana akitaka kuchuana na Rais Kagame.

Mwanasiasa huyo wa upinzani aliye na umri wa miaka 35 na ambaye ni mhasibu kitaaluma amekuwa akimtuhumu Rais Kagame kwamba anawabinya wapinzani; na kukikosoa chama tawala cha RPF kwa kuweko madarakani tangu kiliposhika hatamu za uongozi baada ya kuhitimisha mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.