Dec 06, 2018 14:51 UTC
  • Homa ya Manjano yaua watu 9 nchini Nigeria

Mripuko wa homa ya manjano nchini Nigeria umesababisha vifo vya watu tisa katika jimbo la Edo kusini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kamishna wa Afya katika jimbo hilo, Dakta David Osifo amesema walioaga dunia katika mripuko huo ni vijana waliokuwa na umri wa kati ya miaka 14 na 20, na kwamba saba miongoni mwao waliaga dunia hata kabla ya kufikishwa hospitalini.

Amesema ugonjwa huo kwa sasa umeenea katika miji 10 kati ya 18 ya jimbo hilo, huku Wizara ya Afya ya Nigeria ikitazamiwa kuanza kutoa chanjo na kuchukua hatua za kuidhibiti homa hiyo hatari.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.

 

Mripuko wa homa ya manjano nchini Angola ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 350 kati ya Disemba 2015 na Julai 2016

Mapema mwezi uliopita wa Novemba, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa watu 10 wamepoteza maisha kutokana na Homa ya Manjano kusini magharibi Ethiopia.

Aidha kati ya Disemba mwaka 2016 na tarehe 23 mwezi Aprili mwaka jana, wanawake 25 wajawazito walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, huku kesi 135 zikiripotiwa katika kambi ya wakimbizi eneo la Diffa, kusini mwa Niger. 

 

Tags