Dec 18, 2018 03:26 UTC
  • Boko Haram wafanya shambulizi jingine mashariki mwa Nigeria

Genge la kigaidi na la ukufurishaji la Boko Haram limevamia na kushambulia kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuchoma moto nyumba za wanakijiji baada ya kuwashambulia kwa risasi.

Maafisa wa kijeshi wa Nigeria wamethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mamia ya wakazi wa kijiji cha Maiborti karibu na mji wa Maiduguri wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wamelazimikia kukimbilia upande wa mji huo baada ya magaidi hao kuvamia kijiji chao na kuwachomea moto nyumba zao.

Maafisa hao wamesema, jeshi la Nigeria lililokuwa limejizatiti kwa zana za kivita na kwa kusaidiwa na ndege za kijeshi wamefanikiwa kuwafurusha magaidi hao kwenye kijiji hicho.

Hadi tunapokea habari hii, hakukuwa kumetangazwa habari yoyote kuhusu wahanga wa uvamizi huo.

Eneo la Ziwa Chad ambalo linashuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi wa Boko Haram

 

Genge la ukufurishaji la Boko Haram lilianza kufanya mashambulizi kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009 na tangu wakati huo hadi hivi sasa limeshasababisha zaidi ya watu 20 elfu kuuawa na zaidi ya milioni mbili na laki sita wengine kuwa wakimbizi.

Genge la Boko Haram limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh na limekuwa likifanya mashambulizi katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Chad, Niger na Cameroon.

Nchi hizo nne zimeunda kikosi cha pamoja cha kupambana na magaidi wa Boko Haram lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kuliangamiza genge hilo la wakufurishaji.

Tags