AU yazikosoa nchi za Ulaya zilizokataa kusaini Mkataba wa Wahajiri
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amezikosoa vikali nchi kadhaa za Ulaya zilizokataa kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Wahajiri.
Katika Mkutano wa Afrika na Ulaya wa Kuimarisha Uhusiano wa Kidijitali jana Jumanne mjini Vienna nchini Austria, Moussa Faki Mahamat alisema, "Nilikuwa Morocco hivi karibuni, ambapo nchi nyingi za Ulaya zilikataa kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Wahajiri. Hatupaswi kuacha tofauti zetu za kisiasa zitugawanye."
Amesema changamoto za nchi za bara Afrika haziwezi kutatuliwa kwa ruzuku na misaada tu, lakini kwa kuzungumza na jamii za bara hilo juu ya namna ya kufikia malengo yao, na pia kupewa mafunzo na kuwezeshwa vijana wa nchi za bara hilo.
Zaidi ya nchi 150 duniani ziliunga mkono rasmi Mkataba wa Kimataifa wa Wahajiri katika mkutano uliofanyika nchini Morocco kati ya tarehe 10 na 11 mwezi huu licha ya upinzani mkubwa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Hata hivyo nchi za Ulaya za Poland, Jamhuri ya Czech , Austria, Hungary, Bulgaria, Latvia, Italia na Australia, pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel zilikataa kutia saini mkataba huo; mbali na Marekani ambayo tangu hapo awali ilitangaza kutouunga mkono.
Wadadisi wa mambo wanasema mgogoro mkubwa wa wahajiri na wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa ni matokeo ya siasa za uingiliaji kati za madola ya Magharibi katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika; mgogoro ambao umelihusisha pia bara Ulaya.