Magaidi 14 wauawa kaskazini mwa Misri
(last modified Mon, 24 Dec 2018 08:01:28 GMT )
Dec 24, 2018 08:01 UTC
  • Magaidi 14 wauawa kaskazini mwa Misri

Maafisa usalama wa Misri wametangaza habari ya kuuawa magaidi 14 katika mkoa wa Sinai Kaskazini wa kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Maafisa hao wa Misri wamesema kuwa, vikosi vya serikali vimeshambulia maficho ya magaidi hao katika mji wa al Arish, makao makuu wa mkoa wa Sinai Kaskazini na kuua magaidi 8 katika maficho hayo.

Magaidi wengine 6 wameuawa wakati wakikimbizana na askari wa kupambana na magaidi. Hata hivyo maafisa hao wa serikali ya Misri hawakutoa ufafanuzi zaidi kuhusu wakati yalipofanyika mashambulizi hayo.

Wanajeshi wa Misri

 

Eneo la Sinai la kaskazini mwa Misri limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha dhidi ya wanajeshi na maafisa usalama wa serikali. Mashambulio hayo yameongezeka baada ya rais wa hivi sasa Abdel Fattah el Sisi kushika hatamu za uongozi mwaka 2014 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Mohammad Morsi, rais wa kwanza kabisa kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

Genge la kigaidi la Wilaya ya Sinai, tawi la magaidi wa Daesh (ISIS) ndilo linalofanya mashambulizi mengi katika mkoa wa Sinai Kaskazini huko Misri.