Eneo la Puntland la Somalia lapata rais mpya
Bunge la eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland limemchagua Said Abdullahi Deni kuwa rais eneo hilo, kuchukua nafasi ya Abdiweli Mohamed Ali Gaas.
Deni ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mipango wa Somalia alichaguliwa jana kuwa rais wa Puntland katika kikao cha Bunge, baada ya kupata kura 35 katika duru ya pili ya uchaguzi, huku mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi akipata kura 31.
Rais anayeondoka wa eneo hilo, Abdiweli Mohamed Ali Gaas aliondolewa katika duru ya kwanza ya zoezi hilo lililofanywa na wabunge 66 wa eneo hilo, waliochaguliwa hivi karibuni.
Baada ya kura hiyo, Spika wa Bunge, Abdihakin Mohamed Ahmed alisema, "Namtangaza rasmi, Said Abdullahi Deni kuwa rais mpya wa Puntland kwa muda wa miaka mitano."
Serikali mpya ya Abdullahi Deni itakayokuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa usalama, haswa zimwi la wanamgambo wa al-Shabab.
Mbali na hujuma za al-Shabaab, eneo hilo mara kadhaa limekuwa likishuhudia mapigano baina yake na maeneo jirani. Mwaka 2016, askari wa eneo la Puntland na GalMudug walipambana kwa wiki kadhaa kugombania udhibiti wa eneo lenye utata la Galkayo.
Aidha vikosi vya maeneo yenye mamlaka ya ndani ya Somaliland na Puntland nchini Somalia vilishambuliana na makumi ya watu kuuawa, katika vita vya kung'ang'ania wilaya ya Tuqarak, katika eneo la Sool.