Watu 14 wauawa katika shambulizi la mawahabi Burkina Faso
Jeshi la Burkina Faso limetangaza kuwa, watu wasiopungua 14 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na kundi la kitakfiri na kiwahabi nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Burkina Faso imesema kuwa, watu waliokuwa na silaha wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa kundi lenye misimamo mikali wameua raia 14.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, jeshi limejibu jinai hiyo kwa kushambulia ngome za makundi yenye misimamo mikali katika mikoa mitatu ya kaskazini mwa nchi hiyo. Imesema mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Jeshi la Burkina Faso yameua na kuangamiza wanachama 146 wa makundi ya kitakfiri nchini humo. Hata hivyo habari hii ya mauaji ya zaidi ya wapiganaji 140 wa makundi ya kigaidi nchini Burkina Faso bado haijathibitishwa na vyombo vya kujitegemea.
Katika mwaka mmoja uliopita Burkina Faso imelengwa kwa mshambulizi kadhaa ya kigaidi yaliyoanzia kaskazini mwa nchi hiyo na kisha kuyakumba maeneo ya mashariki na katika mpaka wake na nchi ya Mali. Mengi kati ya mashambulizi hayo yamehusishwa na kundi la kigaidi la al Qaida.