Feb 07, 2019 14:43 UTC
  • Mgogoro wa Burundi umeshindikana? Mkapa alia na EAC kumtelekeza

Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kuna kila dalili za kuonesha kuwa mgogoro wa Burundi umeshindikana kutatuliwa.

Hii ni kwa sababu licha ya marais wa Uganda, Kenya na Tanzania kukabidhiwa majukumu na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza mazungumzo baina ya pande hasimu huko Burundi, lakini hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika juhudu za kutatua mgogoro huo.

Tukio la karibuni kabisa ni hatua ya Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ya kulalamika kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki imemtelekeza katika suala hilo.

Tarehe 31 mwezi uliopita wa Januari 2019, Benjamin Mkapa aliwasilisha ripoti kwa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akisisitiza kuwa serikali ya Burundi na wapinzani wanapaswa kuzungumza na kukubaliana kuhusu mfumo wa kisheria na taratibu zinazohitajika za kufanyika uchaguzi ujao.

Mazungumzo ya amani ya Burundi mjini Entebbe Uganda

 

Katika ripoti yake hiyo, Mkapa ameelezea kusikitishwa na hatua ya serikali ya Burundi ya kususia kikao cha mwisho cha mazungumzo na wapinzani.

Vile vile amelalamika kuwa juhudi zake hazikuungwa mkono inavyotakiwa hasa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Amelalamika kuwa jumuiya hiyo hata imeshindwa kufanya mkutano wa kilele kuhusu mgogoro wa Burundi na hivyo kupelekea akose kuungwa mkono na jumuiya hiyo.

Itakumbukwa kuwa, moja ya mikakati ya rais huyo wa zamani wa Tanzania ni kuweko mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote kulingana na ajenda iliyowekwa katika mazungumzo ya awali na ameomba viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunga mkono juhudi za kufanyika uchaguzi nchini Burundi utakaoungwa mkono na pande zote hasimu.

Tags