Rais Bouteflika kurejea nchini Algeria leo, maandamano yachachamaa
Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria anatazamiwa kurejea katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika leo Jumapili, baada ya kuwa nje ya nchi kwa muda wa wiki mbili kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ndege ya serikali ya Algeria imetua mapema leo katika Uwanja wa Ndege ya Cointrin mjini Geneva nchini Uswisi.
Ndege hiyo ya Gulfstream ndiyo iliyompeleka Bouteflika nchini Uswisi Februari 24 kwa ajili ya matibabu.
Kanali ya televisheni ya Ennahar imeripoti kuwa, rais huyo mkongwe anayeugua ugonjwa wa kiharusi kwa miaka kadhaa sasa anatazamiwa kurudi nchini leo.
Haya yanajiri huku mamia ya maelfu ya wanachuo wakifanya maandamano hii leo katika mji mkuu Algiers, dhidi ya Bouteflika.
Katika kile baadhi ya wadadisi wa mambo wametafsiri kuwa ni kuunga mkono maandamano hayo, Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Luteni Jenerali Gaed Salah hii leo amesema, "Jeshi na wananchi wana muono wa pamoja wa mustakabali wa nchi."
Waalgeria ambao wamechoshwa na uongozi mbovu ambao umesababisha ukosefu wa ajira na ufisadi wamekuwa wakiandamana tokea Februari 22 wakimtaka Bouteflika, mwenye umri wa miaka 82, asitishe mpango wake wa kugombea urais kwa muhula wa tano mfululizo katika uchaguzi wa Aprili 18.