Mar 13, 2019 13:10 UTC
  • Magaidi 33 wa Boko Haram waangamizwa mashariki mwa Niger

Jeshi la Niger limetangaza kuwa, limewaangamiza wanachama 33 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni kabambe ya jeshi hilo kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Niger imeeleza kwamba, kwa akali magaidi 33 wa kundi la Boko Haram wameuliwa katika operesheni ya vikosi vya nchi hiyo katika mji wa Diffa ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo jirani kabisa na mpaka wa Nigeria.

Kadhalika taarifa hiyo imeeleza kuwa, kiwango kikubwa cha silaha na zana za kivita za wanamgambo hao zimetwaliwa na wanajeshi wa Niger. 

Operesheni ya jeshi la Niger ni muendelezo wa operesheni kabambe iliyoanzishwa na jeshi la nchi hiyo juma lililopita yenye lengo la kulisafisha eneo la Ziwa Chad na uwepo wa magaidi hao ambao wamehatarisha amani na usalama wa raia.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hayo yanajiri siku chache tu baada ya magaidi wengine 50 wa Boko Haram kuuawa katika operesheni za kikosi cha pamoja cha Nigeria, Chad, Cameroon na Niger.

Uasi na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambapo hadi sasa yameshasababisha zaidi ya watu elfu ishirini kuuawa na wengine karibu milioni tatu kubaki bila makazi na hivyo kulazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amekuwa akiahidi kila mara kuchukua hatua kali za kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haramu, lakini hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake hiyo

Tags