Maafisa wa chama tawala Algeria wajitenga na Rais Bouteflika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52189-maafisa_wa_chama_tawala_algeria_wajitenga_na_rais_bouteflika
Maafisa waandamizi wa chama tawala nchini Algeria cha FNL wamemtaka Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo kuchukua hatua ya 'kihistoria', hatua nyingine ambayo inaashiria kuwa chama hicho kimeendelea kujiweka mbali na Bouteflika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2019 01:12 UTC
  • Maafisa wa chama tawala Algeria wajitenga na Rais Bouteflika

Maafisa waandamizi wa chama tawala nchini Algeria cha FNL wamemtaka Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo kuchukua hatua ya 'kihistoria', hatua nyingine ambayo inaashiria kuwa chama hicho kimeendelea kujiweka mbali na Bouteflika.

Hocine Kheldoun, msemaji wa zamani wa FNL ameiambia kanali ya televisheni ya Ennahar kuwa, aghalabu wa maafisa wa chama hicho wamepiga darubini na kuona kwamba, kuna haja na kuegemea upande wa wananchi waliowengi.

Jana Ijumaa, maelfu ya wananchi wa Algeria wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa chama tawala na wanafunzi wa vyuo vikuu walimiminika mitaani na kufanya maandamano dhidi ya Bouteflka, licha ya kiongozi huyo kulazimika kukubali matakwa yao na kutangaza kuwa hatagombea tena kiti cha rais.

Madjid Benzida, kijana mwenye umri wa miaka 37 ambaye alishiriki maandamano ya jana alisema, "Wale wanaodhani kuwa tumechoka wanakosea. Hatutasitisha maandamano hadi tufikie malengo yetu."

Waalgeria wamesema wamechoshwa na utawala wa Bouteflika, ambaye yuko madarakani tokea mwaka 1999

Jumatatu iliyopita Rais Abdelaziz Bouteflka alifutilia mbali azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi ujao na kusema kuwa, uchaguzi huo uliotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Aprili utasogezwa mbele kidogo kwa ajili ya kutoa fursa ya kufanyika Kongamano la Kitaifa kuhusu mustakabali wa kisiasa nchini humo.

Rais Abdelaziz Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.