Maafisa wa Tume ya Uchaguzi DRC wakanusha madai ya ufisadi ya Marekani
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI, Corneille Nangaa pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa tume hiyo wamekanusha vikali madai ya Marekani kwamba walihusika katika ufujaji wa fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi uliopita nchini humo.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Nangaa amekanusha tuhuma hizo zilizotolewa na maafisa wa Washington na kubainisha kuwa: "Sijawahi kujihusisha na aina yoyote ya ufisadi. Tulifuata kanuni za Bodi (ya Tume ya Uchaguzi), na maelekezo ya Bunge."
Ijumaa iliyopita, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo Mwenyekiti wa CENI na maafisa hao wawili wakuu wa tume hiyo, mbali na kuzuia mali zao zilizoko nchini humo kwa tuhuma hizo za ufisadi na eti kupindisha mkondo wa demokrasia nchini humo.
Mbali na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Corneille Nangaa, wengine waliokanusha madai hayo ya ufisadi ya Marekani ni Naibu Mwenyekiti wa CENI, Norbert Basengezi na Marcellin Mukolo Basengezi, mtoto wa kiume wa naibu mwenyekiti ambaye ni mshauri wa Nangaa.
Katika uchaguzi huo wa Disemba mwaka jana, Tume ya Uchaguzi CENI, ilimtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kuzoa asilimia 38 ya kura, huku mpinzani wake wa karibu Martin Fayulu akipata asilimia 34.
Hata hivyo Fayulu na Kanisa Katoliki nchini humo walidai kuwa uchaguzi huo ulizungukwa na uchakachuaji wa matokeo kwa maslahi ya Tshisekedi.