Hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52591-hatimaye_rais_abdelaziz_bouteflika_wa_algeria_ajiuzulu
Hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amejiuzulu wadhifa wake baada ya miaka 20 kufuatia wiki kadhaa za maandamano na mashinikizo dhidi yake.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 02, 2019 22:57 UTC
  • Hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ajiuzulu

Hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amejiuzulu wadhifa wake baada ya miaka 20 kufuatia wiki kadhaa za maandamano na mashinikizo dhidi yake.

Abdelaziz Bouteflika ambaye amekuwa madarakani kama rais wa Algeria kwa muda wa miaka 20, tayari alikuwa amefutilia mbali mpango wake wa kugombea muhula mwingine baada ya kushadidisha mashinikizo dhidi yake.

Aidha wiki iliyopita Mkuu wa Majeshi nchini Algeria Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah  alilitaka Baraza la Katiba la nchi hiyo kutumia kifungu nambari 102 cha Katiba ya nchi na kutangaza kuwa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi kama Rais.

Mnamo mwezi Februari mwaka huu, Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni mgonjwa alitangaza kuwa atagombea tena urais kwa muhula wa tano mfululizo.

Kutangazwa habari hiyo kulizusha wimbi la malalamiko makubwa na upinzani mkali wa wananchi na kumfanya kiongozi huyo abadilishe uamuzi wake.

Hatimaye maandamano ya wananchi wa Algeria yaliyokuwa yakimshinikiza Abdelaziz Bouteflika alijizulu yamezaa matuunda

Bouteflika (82) amekuweko madarakani nchini Algeria tangu mwaka 1999 yaani miaka 20 iliyopita na mara zote alikuwa akigombea urais na kutangazwa mshindi katika vipindi vinne vya miaka mitano mitano vilivyopita.

Abdelaziz Bouteflika ambaye anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, amekuwa akionekana hadharani kwa nadra sana tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.