Furaha, nderemo na vifijo vyatanda nchini Algeria baada ya Bouteflika kujiuzulu
Miji mbalimbali ya Algeria imeendelea kushuhudia furaha, nderemo na vifijo baada ya Rais Abdelaziz Bouteflika kutangaza kujiuzulu.
Wananchi wa miji mbalimbali ya Algeria ukiwemo mji mkuu Algiers wameendelea kumiminika katika barabara na mitaa wakishangilia na kusherehekea kujiuzulu Abdelaziz Bouteflika aliyeiongoza nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika tangu mwaka 1999.
Jana Rais Abdelaziz Bouteflika aliyeiongoza Algeria kwa muda wa miaka 20 alikabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa Baraza la Katiba la nchi hiyo na hivyo kuhitimisha uongozi wake wa miongo miwili.
Wiki iliyopita Mkuu wa Majeshi nchini Algeria Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah alilitaka Baraza la Katiba la nchi hiyo kutumia kifungu nambari 102 cha Katiba ya nchi na kutangaza kuwa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi kama Rais.
Mnamo mwezi Februari mwaka huu, Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni mgonjwa alitangaza kuwa atagombea tena urais kwa muhula wa tano mfululizo.
Kutangazwa habari hiyo kulizusha wimbi la malalamiko makubwa na upinzani mkali wa wananchi na kumfanya kiongozi huyo abadilishe uamuzi wake.
Abdelaziz Bouteflika ambaye anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, amekuwa akionekana hadharani kwa nadra sana tangu alipopatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.