Kujiuzulu Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria na mustakabali wa nchi hiyo
Hatimaye Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria amejiuzulu wadhifa wake baada ya miaka 20 kufuatia wiki kadhaa za maandamano na mashinikizo dhidi yake. Bouteflika alitangaza uamuzi huo jana Jumanne na kusema amelijulisha Baraza la Katiba kuhusu hatua yake ya kujiondoa madarakani.
Wiki iliyopita Mkuu wa Majeshi nchini Algeria Luteni Jenerali Ahmed Gaid Salah alilitaka Baraza la Katiba la nchi hiyo kutumia kifungu nambari 102 cha Katiba ya nchi na kutangaza kuwa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya uongozi kama Rais.
Bouteflika pia amejiuzulu baada ya maandamano ya wiki kadhaa ya wananchi ambao walimtaka anondoke madarakani na kuandaliwe mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki.
Hivi sasa matukio ya kisiasa ya Algeria yanaingia awamu mpya baada ya kujiuzulu Bouteflika. Hata kama awali idadi kubwa ya waandamanaji walikuwa wanamkata Bouteflika ajiuzulu kutokana na udhaifu wa kimwili na si sera zake, lakini sasa Waalgeria walio wengi wamebainishwa wazi kuwa hawaridhishwi na hali ya sasa ya nchi yao na wanataka mabadliko ya kimsingi katika mfumo wa kisiasa.
Hivi sasa mustakabali wa Algeria hauko wazi. Kwa mujibu wa katiba ya Algeria, baada ya kujiuzulu Bouteflika, kama rais Spika wa Bunge la Kitaifa Abdelkader Bensalah anapaswa kuchukua nafasi ya rais wa muda kwa kipindi cha siku tisini kabla ya uchaguzi kufanyika. Yeye ni kati ya wanasiasa watiifu kwa Boutefklika na alikuwa anaunga mkono uamuzi wake wa kugombea urais wa muhula wa tano na kwa msingi huo vyama vya upinzani na waandamanaji wanasema Abdelkader Bensalah si chaguao bora la rais wa muda kwani ataendeleza mfumo ulioko wa kisiasa.
Katika upande wa pili, wengi wana hofu kuwa iwapo jeshi litachukua madaraka na nchi hiyo itaelekea katika udikteta wa kijeshi. Hatahivyo Mkuu wa Majeshi ya Algeria amesema jeshi halina nia ya kutwaaa madaraka. Mkuu wa Majeshi ya Algeria Ahmed Gaid Salah ambaye alipendekeza kutumika kifungu cha 102 cha katiba katika kumuuluzu Bouteflika, ameahidi kuwa wananchi ndio watakao kabidhiwa madaraka na kwamba binafsi hatashiriki katika uchaguzi. Aidha ameahidi kuwa, watuhumiwa wote wa ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma watakamatwa.
Bouteflika katika tangazo lake la kujiuzulu alisema kabla ya kuondoka madarakani kumechukuliwa maamuzi muhimu. Lakini hadi sasa haijulikani ni maamuzi yapi aliyoyachukua. Lakini vyama vya upinzani Algeria vimetangaza kuwa, vitapinga kila aina ya uamuzi au taarifa kutoka ofisi ya rais wa Algeria.
Chama cha mrengo wa kushoto Algeria kimeashiria maudhui hiyo na kusema jitihada za serikali ya mpito za kujaribu kusafisha tasiwra ya mfumo wa sasa hazina maana. Ukweli ni kuwa waliowengi wanataka kuona mfumo wote uliofungamana na Bouteflika ukiondoka kwani hauna ustahiki wa kutawala.
Ni wazi kuwa mustakabali wa kisiasa wa Algeria kwa sasa umejaa kiza. Kuna wale wasemao kuwa waliobaki katika utawala wa Bouteflika watajaribu kujipanga tena ili wachukue tena uongozi huku wengine wakisema kuwa hivi sasa kutashuhudiwa mabadiliko ya kimsingi katika mafumo wa utawala kwa mujibu wa matakwa ya wananchi.