Guterres: Kuna haja ya kuunganishwa taasisi za Libya kabla ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52621-guterres_kuna_haja_ya_kuunganishwa_taasisi_za_libya_kabla_ya_uchaguzi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitembelea Libya siku chache kabla ya kufanyika kongamano la kitaifa la kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2019 03:29 UTC
  • Guterres: Kuna haja ya kuunganishwa taasisi za Libya kabla ya uchaguzi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitembelea Libya siku chache kabla ya kufanyika kongamano la kitaifa la kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi nchini humo.

Antonio Guterres aliitembelea Libya jana Jumatano na kuandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Nimewasili Libya, nimejitolea kwa dhati kuunga mkono mchakato wa kisiasa utakaoongozwa na Walibya wenyewe, na ambao utapelekea kupatikana amani, uthabiti, demokrasia na mafanikio kwa ajili ya watu wote wa Libya."

Guterres ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa UN kuitembelea nchi hiyo ya kaskizini mwa Afrika tokea mwaka 2014, amesema kuna haja ya kuziunganisha taasisi za uongozi nchini humo, ili kuepuka migogoro zaidi na kuirejesha Libya katika hali ya uthabiti.

Mkutano huo wa kujadili uchaguzi ujao nchini Libya na utakaozijumuisha pande zote za kisiasa, unatazamiwa kufanyika kati ya Aprili 14 na 16 magharibi mwa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.

Libya mbali na mgogoro wa kisiasa, inakabiliwa pia na mashambulizi ya magenge ya kigaidi

Awali uchaguzi mkuu nchini humo ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 10 mwaka jana 2018 lakini zoezi hilo liliahirishwa kutokana mpasuko uliojitokeza baina ya viongozi wa mirengo hasimu ya kisiasa na wimbi la mapigano na machafuko yaliyozuka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.