Apr 12, 2019 15:00 UTC
  • 'Al-Shabaab' yawateka nyara madaktari 2 wa Cuba nchini Kenya

Watu waliojizatiti kwa silaha wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wamewateka nyara madaktari wawili wa Cuba katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Msemaji wa Polisi nchini Kenya, Charles Owino amesema wanamgambo hao waliokuwa kwenye magari mawili aina ya Toyota Probox mapema leo walilisimamisha gari lililokuwa limewabeba madaktari hao katika mji wa Mandera, eneo la kaskazini mashariki mwa nchi na kisha wakaanza kulifyatua risasi, ambapo afisa mmoja wa polisi aliyekuwa anawalinda madaktari hao ameuawa.

Ameongeza kuwa, afisa mwingine wa polisi amejeruhiwa katika makabiliano hayo. 

Duru za habari zinaarifu kuwa, madaktari hao wa Cuba walikuwa wanaelekea kazini wakati wa shambulizi hilo linaloaminika kufanywa na wanamgambo wa al-Shabaab, wanaodaiwa kupenya nchini Kenya wakitokea Somalia.

Msemaji wa Polisi nchini Kenya amebainisha kuwa, dereva wa madaktari hao ametiwa mbaroni kwa ajili ya kulisaidia jeshi la polisi katika uchunguzi.

Wanachama wa genge la ukufurishaji la al-Shabaab

Itakumbukwa kuwa, mwezi Mei mwaka jana wa 2018, madaktari zaidi ya 100 kutoka Cuba waliwasili Kenya na kutumwa katika kaunti zote 47 kupiga jeki sekta ya afya nchini humo.

Aidha madaktari wapatao 50 kutoka Kenya walielekea Cuba mwezi Septemba mwaka huo kwa ajili ya mafunzo ya miaka miwili.

Tags