Watu 80 wakamatwa kwa kula mchana wa Ramadhani jimboni Kano, Nigeria
Polisi wanaosimamia sheria za Kiislamu (Sharia) katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria wamewatia mbaroni watu 80 kwa tuhuma za kula mchana hadharani, wakati huu wa funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Polisi hao ambao wanafahamika kama 'Hisbah' wameeleza kuwa watu hao wamekamatwa katika maeneo mbalimbali kwenye jiji la Kano ndani ya kipindi cha siku chache zilizopita.
Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo yanafuata sheria za Kiislamu tangu mwaka 2000, lakini wanazingatia pia sheria za nchi.
Msemaji wa Polisi ya Hisbah katika jimbo hilo, Adamu Yahaya amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, watu hao waliokamatwa ni Waislamu na kwamba maafisa wa jeshi hilo hawawakamati watu ambao sio waumini wa dini hiyo kwa kuwa sheria za Kiislamu haziwahusu.

Amesema kuwa baadhi ya watu waliokamatwa waliwaambia maafisa wa polisi kuwa walikuwa wanakula kwa sababu wao binafsi hawakuuona mwezi ukiandama, na wengine walitoa sababu za ugonjwa ambazo zilionekana kuwa hazina mashiko.
Hata hivyo, Yahaya amesema kuwa watu hao wote 80 waliachiwa huru kwa sababu walibainika kuwa walifanya kosa hilo kwa mara ya kwanza.
Hisbah wameeleza kuwa wataendelea na msako wao katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na watawakamata Waislamu wote ambao hawafuati masharti ya kufunga katika kipindi hiki bila kuwa na sababu za msingi.