Daesh yatangaza kuhusika na mauaji ya askari 28 wa Niger
(last modified Fri, 17 May 2019 07:34:02 GMT )
May 17, 2019 07:34 UTC
  • Daesh yatangaza kuhusika na mauaji ya askari 28 wa Niger

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na shambulio dhidi ya msafara wa magari ya jeshi la Niger na kuua askari 28 wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kundi hilo la ukufurishaji lilikiri kuhusika na hujuma hiyo ya kuvizia jana Alkhamisi bila kutoa ushahidi wala ufafanuzi wa kina. Magaidi hao wamesema mbali na shambulio hilo la Jumanne karibu na mpaka wa Mali, lilitekeleza pia hujuma nyingine dhidi ya gereza siku chache zilizopita nchini Mali.

Shambuo hilo la Jumanne lilitokea karibu na eneo la Mangaize, yapata kilomita 45 kutoka eneo la Tongo Tongo, ambapo genge hilo liliua wanajeshi wanne wa Marekani Oktoba mwaka 2017.

Niger ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani inaandamwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na magenge ya ndani na nje ya nchi.

Askari wanne wa Marekani waliouawa nchini Niger Oktoba 2017

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, watu 10 waliuawa katika shambulizi la bomu la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram mashariki mwa Niger.

Kundi hilo la wakufurishaji limekuwa likifanya mashambulizi ya kikatili katika nchi hiyo na majirani zake Nigeria, Chad na Cameroon, mashambulio ambayo hadi hivi sasa yameshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hizo za Afrika Magharibi.

Tags