UN yamteua afisa kupambana na Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Umoja wa Mataifa umemteuwa Mratibu wa Hatua za Dharura za Kukabiliana na Maradhi ya Ebola ambaye atasaidia kuimarisha jitihada za kukomesha kuenea maradhi ya Ebola yaliyodumu kwa miezi kumi sasa huko Kongo DRC na kuua watu zaidi ya 1,200.
Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimesema leo katika taarifa yao kuwa, David Gressly ameteuliwa kushika wadhifa huo mpya. Taarifa ya taasisi hizo mbili imeongeza kuwa, Gressly atakuwa na jukumu la kusimamia uratibu wa misaada ya kimataifa kwa ajili ya uchukuaji hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa yanakuwepo mazingira mazuri ya kiusalama na kisiasa ili kuruhusu kuchukuliwa hatua zinazopasa katika kushughulikia maradhi ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa, haiwezekani kudhibiti maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na yamkini maafa ya ugonjwa huo yakawa makubwa zaidi kuliko yale yaliyoshuhudiwa magharibi mwa Afrika mwaka 2013 na 2016. Ripoti zinaonyesha kuwa, katika miezi ya hivi karibuni kesi za maambukizi ya maradhi ya Ebola zimeongezeka sana na kwamba, hakuna dalili za kupungua maradhi hayo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, juhudi za kukabiliana na maradhi ya Ebola katika Jamhuri yya Kidemokrasia ya Congo zinakabiliwa na changamoto kubwa ambayo ni mashambulio ya makundi ya wanamgambo dhidi ya madakatri wanaojihusisha na harakati za kutibu raia wanaougua maradhi hayo.