Waislamu wazidi kuandamana Nigeria kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky
Maelfu ya wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja kushinikiza kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Televisheni ya Press TV imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, waandamanaji hao wamesema kuwa, kuendelea kumshikilia korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru, ni jambo linalopaswa kulaaniwa kabisa.
Waandamanaji hao wameongeza kuwa, kwa mujibu wa ripoti za madaktari wa kamisheni ya haki za binadamu ya Kiislamu yenye makao yake mjini London Uingereza, Sheikh Zakzaky inabidi awe karibu na uangalizi wa madaktari hasa baada ya kupigwa risasi kadhaa na wanajeshi wa Nigeria.
Abdullahi Muhammad Musa, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo amesema kuwa, vyombo vya kuaminika vimetahadharisha kuwa Sheikh Zakhzaky na mkewe wanahitajia sana misaada ya matibabu njeya jela vinginevyo watapata madhara makubwa wakiendelea kushikiliwa korokoroni hasa kwa vile walipigwa risasi kadhaa na wanajeshi wa nchi hiyo.
Tarehe 13 Disemba 2015 wanajeshi wa Nigeria walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu baada ya kuivamia Husainia ya mji wa Zaria na kuwaua kiholela Waislamu hao ikiwa ni pamoja na kuwapiga risasi Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe. Taarifa zinasema kuwa risasi hizo zimepelekea Sheikh Zakzaky apoteze jicho lake moja huku mamia ya Waislamu wakiuawa kwa risasi wakiwemo watoto watatu wa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.