Mmoja auawa, 10 wajeruhiwa kwa risasi za polisi nchini Sudan + Video
Habari kutoka nchini Sudan zinasema kuwa polisi wa jeshi wamewashambulia kwa risasi wananchi walioendeleza maandamano na kukusanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo katika mji mkuu Khartoum na kumuua kijana mmoja wa miaka 20 na kujeruhi wengine 10.
Televisheni ya "Rusia al Yaum" imetangaza habari hiyo na kuinukuu Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ikisema leo Jumapili kwamba, mbali na watu hao 11 waliouawa na kujeruhiwa, watu wengine kadhaa wamepigwa marungu na kugongwa na magari ya polisi na kuumizwa vibaya.
Televisheni hiyo imeongeza kuwa, ufyatuaji risasi ulitokea baada ya polisi wa Sudan kujaribu kuondoa vizuizi vya barabarani vilivyokuwa vimewekwa na wananchi hao wanaolalamikia jeshi kung'ang'ania madaraka ya nchi.
Makundi ya upinzani yamelaani vikali hatua hiyo ya polisi wa jeshi la Sudan na kusema kuwa wataendelea kupania utawala wa raia hata kama wanajeshi watazidi kuwakandamiza.
Makundi mawili ya Sudan yaani Jumuiya ya wafanyakazi wa Sudan na kamati ya uchukuaji hatua ya "Muungano wa Makundi ya Ukombozi na Mabadiliko" ambao ndio muungano mkubwa zaidi wa wapinzani huko Sudan yametoa taarifa tofauti na kulaani hatua ya jeshi la Sudan ya kuwashambulia kwa risasi waandamanaji, kufanya mauaji, kuwagonga kwa magari na kuwapiga marungu raia wanaoandamana kwa amani yakisisitiza kuwa, lengo la wanajeshi hao wa Sudan lilikuwa ni kuua.
Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan limeonya kuhusu kuundwa serikali ya kiraia nchini humo hivi sasa na kudai kuwa, jambo hilo litazidisha machafuko nchini humo.