Maelfu waandamana Algeria wasema ,'Nyote Ondokeni'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53990-maelfu_waandamana_algeria_wasema_'nyote_ondokeni'
Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Algeria, Algiers wakitaka rais wa mpito Abdlekader Bensalah aondoke baada ya sisitizo lake kuwa atabakia madarakani hadi rais mpya achaguliwe.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jun 08, 2019 03:11 UTC
  • Maelfu waandamana Algeria wasema ,'Nyote Ondokeni'

Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Algeria, Algiers wakitaka rais wa mpito Abdlekader Bensalah aondoke baada ya sisitizo lake kuwa atabakia madarakani hadi rais mpya achaguliwe.

Huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa maneno ya, 'Nyote Ondokeni' na 'Tunataka Viongozi Wapya', waandamanaji walimiminika katikati mwa Algiers kwa Ijumaa ya 16 mfululizo wakitaka maafisa wote wa utawala waondoke madarakani.

Hivi karibuni Baraza la kikatiba nchini Algeria limetangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Julai 4 na kusema sababu ya uamuzi huo ni ukosefu wa wagombea. Uamuzi huo utapelekea kuongezeka muda wa mpito wa kisiasa jambo ambalo yamkini likaibua hasira zaidi za waandamanaji.

Kufuatia uamuzi huo, yamkini rais wa muda Abdelkader Bensalah akaongezewa muda wa kubakia madarakani hadi atakapochaguliwa rais mpya.

Abdelaziz Bouteflika

Abdelaziz Bouteflika alilazimika kujiuzulu kama rais wa Algeria kufuatia maandamano makubwa ya wananchi miezi miwili iliyopita baada ya kutawala kwa muda wa miaka 20.

Algeria hivi sasa inashuhudia mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo, mabadiliko ambayo ni natija ya maandamano mtawalia ambayo yamekuwa yakifanywa na Waalgeria tangu Februari 22 mwaka huu. Waalgeria sasa wanataka mabadiliko kamili ya kisiasa huku wakisisitiza kuwa wale wote wanaofungamana na utawala wa Bouteflika wanapaswa kuachia ngazi.

Itakumbukwa kuwa wananchi wa Algeria walikuwa wakilalamikia hatua ya rais wa zamani wa nchi hiyo ya kugombea kwa muhula wa tano mtawalia. Maandamano yalishtadi nchini humo kupinga hatua hiyo na hatimaye Bouteflika akalazimika kujiuzulu kiti cha urais.