Ripoti: Israel ilifanya ujasusi kwa niaba ya Kabila wa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54050-ripoti_israel_ilifanya_ujasusi_kwa_niaba_ya_kabila_wa_drc
Uchunguzi uliofanywa na kanali moja ya televisheni ya Israel umefichua kuwa, shirika la kijasusi la utawala huo haramu la 'Black Cube' lilikodiwa na aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila kwa ajili ya kufuatilia nyendo za wapinzani na wakosoaji wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2019 02:49 UTC
  • Ripoti: Israel ilifanya ujasusi kwa niaba ya Kabila wa DRC

Uchunguzi uliofanywa na kanali moja ya televisheni ya Israel umefichua kuwa, shirika la kijasusi la utawala huo haramu la 'Black Cube' lilikodiwa na aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila kwa ajili ya kufuatilia nyendo za wapinzani na wakosoaji wake.

Televisheni ya Uvda imenukuu mmoja wa majasusi wa zamani wa shirika hilo la Kizayuni ambaye amesema Kabila aliwapa kazi ya kufuatilia mikutano, mikakati na harakati zote za wapinzani na wakosoaji wake.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mkurugenzi wa shirika binafsi la kijasusi la utawala huo haramu la Black Cube, Dan Zorella alikutana na Kabila mwishoni mwa mwaka 2015, na kikao hicho kilikuwa moja ya vikao vilivyozalisha operesheni iliyopewa jina la 'Coltan' iliyokusudia kukusanya taarifa za kintelijensia kutoka kwa waliokuwa wanapinga na kukosoa utawala wa Kabila kipindi hicho.

Televisheni hiyo ya Kizayuni imeripoti kuwa, Kabila alikodi shirika hilo la kijasusi la Israel ambalo pia linafahamika kama 'Mamluki wa Karne ya 21' kwa ajili ya kuwafuatilia pia watu wa karibu wa familia yake ambao hakuwa na imani nao. 

Maafisa usalama DRC wakikabiliana na wapinzani wa Kabila

Uamuzi wa Kabila wa kukataa kung'atuka madarakani baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika Disemba 2016 kilichochea maandamano kadhaa ya upinzani na kusababisha makumi ya watu kuuawa mbali na kushajiisha uasi wa makundi yanayobeba silaha katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ilitoa taarifa kadhaa kulaani mauaji na ukandamizaji huo dhidi ya wapinzani uliofanywa na maafisa usalama katika enzi za Kabila.